Wednesday 19 June 2013

Mtuhumiwa mauaji ya Padri Mushi azidi kusota rumande


 
Na Mauwa Mussa,  (email the author)

Posted  Jumatatu,Juni17  2013  saa 20:33 PM
Kwa ufupi
  • Mahakama hii haichukui vielelezo vya barua za nje ya chombo hiki. Mtu anayeweza kusema kila kitu ni mkurugenzi wa mashtaka, yeye ndiye mwenye dhamana ya kuondoa kesi mahakamani


Zanzibar. Mahakama Kuu ya Zanzibar, imekataa kumwachia kwa dhamana, mshtakiwa Omar Mussa Makame, anayekabiliwa na shtaka la kumuua Padri Evarist Mushi wa Kanisa Katoliki.
Hatua hiyo ilifanywa jana na Jaji Mkuza Issac Sepetu, baada ya upande wa utetezi katika kesi hiyo ,kuiomba mahakama imwachie kwa dhamana mshtakiwa hadi hadi hapo upande wa mashtaka, utakapokamilisha upelelezi.
Alisema mahakama itaendelea na kesi isiyokuwa na dhamana na ambayo upelelezi wake unaweza kuchukua hadi miezi tisa.
Jaji huyo alisema mahakama haifanyi kazi zake kwa kuzingatia taarifa za watu au magazeti yaliyoko nje yake.
“Mahakama hii haichukui vielelezo vya barua za nje ya chombo hiki. Mtu anayeweza kusema kila kitu ni mkurugenzi wa mashtaka, yeye ndiye mwenye dhamana ya kuondoa kesi mahakamani,” alisema Jaji Sepetu.
Baada ya msimamo huo, wakili Abdallah Juma anayemtetea mshtakiwa, aliiomba mahakama iuamuru upande wa mashtaka ,kuharakisha upelelezi wa kesi hiyo.
Alisema ni vyema upande huo ukatoa muda maalum wa kukamilisha upelelezi huo.
Jaji aliipanga kesi hiyo kutajwa tena Julai 2 mwaka huu.
Omar ambaye ni mkazi wa Mwanakwerekwe, Mjini Magharibi, anadaiwa kumuua kwa kumpiga risasi Padri Mushi Februari 17 mwaka huu.

Chanzo: mwananchi news paper