Saturday 15 June 2013

MREMA AKABIDHI URAIS KWA LOWASSA 2015

 

Augustine Mrema (kushoto) na Edward Lowassa.
Mwenyekiti wa TLP, Augustine Mrema amesema biashara ya kugombea urais mwaka 2015 haiwezi kamwe na ametaka ifanywe na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa.

Mrema alisema hayo jana kabla ya harambee ya Saccos ya Walimu wa Wilaya ya Moshi Vijijini, iliyoongozwa na Lowassa katika uwanja wa Ushirika mjini hapa.
Alisema kugombea urais mwaka 2015 ni biashara kubwa kwake kwani amezoea kufanya biashara ndogo ya rejareja yaani ubunge na kumwomba Mungu mwaka huo ufike kwani atakuwa tayari kumwunga mkono Lowassa kwenye kinyang’anyiro hicho.
‘’Nasema biashara ya urais ni biashara kubwa kwangu kwa sasa na biashara hiyo namwachia Lowassa na niko tayari kumwunga mkono kwa hali na mali,’’ alisema Mrema.
Mrema kwa kauli hiyo alishangiliwa na umati wa walimu katika uwanja huo na kusema anamheshimu Lowassa kwa uchapakazi wake uliotukuka.
Alisema viongozi wa aina ya Lowassa ni wachache katika nchi hii na penye ukweli “tunapaswa kuusema” hivyo atamwunga mkono mwaka 2015 kwani yeye atajitoa. 
Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba alisema na kukumbushia kipindi cha uwaziri mkuu wa Lowassa alikuwa akichukua uamuzi wa papo hapo wa kujenga nchi.
Makamba alisema na kueleza kuwa ujasiri wa aina hiyo ya Lowassa, umekuwa adimu kwa muda mrefu hivyo kusema kitendo cha walimu kumkaribisha Lowassa kama mgeni rasmi hawakukosea hata kidogo.
‘’Ninaunga mkono kwa kumkaribisha Lowassa kuwa mgeni wenu rasmi kwani hamkufanya makosa na mnatakiwa kuendeleza mema ambayo ataanzisha hapa,’’ alisema.
Peter Serukamba, Mbunge wa Kigoma Mjini (CCM) alisema bila walimu hakuna maendeleo  nchini hivyo “sote tunapaswa kuwaunga mkono kwa mustakabali wa nchi na si vinginevyo.”
Serukamba alisema yanayofanywa na walimu wa Moshi Vijijini yanapaswa kuigwa na walimu wote nchini kwani ni maendeleo tosha ya kujikwamua kiuchumi.