Monday 17 June 2013

DPP kukata rufaa kupinga dhamana ya Lwakatare Mahakama Kuu

 
Lwakatare (anayeonyesha alama ya V) na mfuasi wake mahakamani. 
Na James Magai na Tausi Ally, Mwananchi  (email the author)

Posted  Jumatatu,Juni17  2013  saa 8:42 AM
Kwa ufupi
 Katika maombi hayo, DPP anaiomba  mahakama hiyo iitishe majalada ya kesi hiyo na kuchunguza uhalali wa uamuzi wa Mahakama Kuu, uliotolewa na Jaji Lawrence Kaduri, kuwafutia washtakiwa hao mashtaka ya ugaidi.

Ni ile ya kuachiwa huru pamoja na kufutiwa mashtaka yaliyokuwa yakimkabili ya ugaidi.
Dar es Salaam. Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) amezidi kumng’ang’ania Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Wilfred Lwakatare (pichani) baada ya kuanza mchakato wa kupinga dhamana yake.
Lwakatare, ambaye anakabiliwa na kesi ya jinai pamoja na mwenzake Ludovick Joseph Rwezaura katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, aliachiwa huru kwa dhamana Juni 11, mwaka huu, baada ya kusota rumande kwa miezi miwili na siku 23.  
Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, Aloyce Katema anayesikiliza kesi hiyo,alimwachia huru kwa dhamana Lwakatare, baada ya Mahakama Kuu, Dar es Salaam kuwafutia mashtaka ya ugaidi yaliyokuwa yakiwabili.
Hata hivyo DPP amewasilisha katika Mahakama ya Kisutu taarifa ya kusudio la kukata rufaa katika Mahakama Kuu, kupinga uamuzi wa Mahakama ya Kisutu kumpa dhamana.   Mbali na taarifa hiyo ya kusudio la kukata rufaa kupinga dhamana yake, DPP pia tayari ameshawasilisha katika Mahakama ya Rufani, maombi ya marejeo ya uamuzi wa Mahakama Kuu kuwafutia mashtaka ya ugaidi.
  Katika maombi hayo, DPP anaiomba  mahakama hiyo iitishe majalada ya kesi hiyo na kuchunguza uhalali wa uamuzi wa Mahakama Kuu, uliotolewa na Jaji Lawrence Kaduri, kuwafutia washtakiwa hao mashtaka ya ugaidi.
 Anadai kuwa katika hati ya maombi ya washtakiwa hao waliyowasilisha Mahakama Kuu, hapakuwapo na maombi ya kufuta mashtaka, na kwamba hapakuwa na taarifa zilizowasilishwa dhidi ya washtakiwa ambazo Mahakama Kuu ingezingatia katika kuamua kama ni halali au la. Hata hivyo Lwakatare kupitia wakili wake, Peter Kibatala kwa niaba ya jopo la mawakili wenzake, amewasilisha pingamizi la awali dhidi ya maombi hayo, akianisha hoja mbili, ambazo mawakili wake watazitoa wakati wa usikilizwaji wa maombi hayo.
  Anadai kuwa maombi hayo ya marejeo yana dosari ambazo haziwezi kurekebishwa kutokana na kushindwa kuambatanisha nakala ya mwenendo wa uamuzi unaolalamikiwa ambao ndiyo maombi hayo yamejengwa na kwamba kiapo kinachounga mkono maombi hayo kimehusisha mambo mengine yasiyohusika
  Kabla ya kufutiwa mashtaka ya ugaidi washtakiwa hao walikuwa wakikabiliwa na mashtaka manne, matatu kati yake yakiwa ya ugaidi na moja la kawaida la jinai, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakidaiwa kula njama na kupanga kumteka Mhariri wa gazeti la Mwananchi Dennis Msacky na kisha kumdhuru kwa kutumia sumu.
  Walipandishwa kizimbani mahakamani hapo kwa mara ya kwanza, Machi 18, mwaka huu na kusomewa mashtaka hayo na kukana baada ya kutakiwa na mahakama hiyo kujibu,licha ya kwamba hawakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa mashtaka hayo husikilizwa na Mahakama Kuu tu.
  Kutokana na mazingira hayo, mawakili wake walimwombea dhamana, lakini siku ambayo Hakimu Emillius Mchauru alitarajia kutoa uamuzi wa maombi hayo ya dhamana, DPP aliwasilisha hati ta kuwafutia mashtaka.