Thursday 30 May 2013

Habari njema : Serikali yapandisha mishahara sekta binafsi

 
Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka akijibu hoja za wabunge waliochangia makadirio ya matumizi ya Wizara yake kwa mwaka 2013/14, bungeni Dodoma, jana. 
Picha na Emmanuel Herman  

Dodoma. Wizara ya Kazi na Ajira imetangaza kuongeza mishahara kwa sekta binafsi kwa kati ya asilimia 20 hadi 65, huku ikikusudia kuongeza nafasi za ajira zaidi ya 300,000 kwa mwaka 2013/14 na kujenga mazingira mazuri kwa ajira binafsi kupitia miradi mbalimbali.
Akitoa makadirio ya matumizi ya wizara yake kwa mwaka 2013/14 jana, Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka alisema wizara imekamilisha utafiti na majadiliano ya kima cha chini cha mshaharakatika sekta binafsi 12.

 
Kabaka alizitaja sekta hizo pamoja na viwango kwa asilimia vya kupandisha mishahara ya kima cha chini ni Viwanda na Biashara (asilimia 43) na Hoteli na Huduma za Majumbani (asilimia 55.2).
Sekta nyingine alizitaja kuwa ni Ulinzi Binafsi ( asilimia 46.4), Madini (asilimia 25.2), Afya (asilimia 65), Uvuvi na Huduma za Majini (asilimia 21.2), Usafirishaji (asilimia 49) na Kilimo (asilimia 46.4).
Kabaka alisema kuwa wakati wowote kuanzia sasa watatangaza viwango halisi vya mishahara kwa sekta hizo, baada ya kazi ya ukokotoaji kukamilika.
“Sekta nyingine mpya ambazo ni Ujenzi, Shule Binafsi, Nishati na Mawasiliano nazo zimepandishiwa viwango,” aliongeza Kabaka.
Katika hatua nyingine, Kabaka alisema katika kipindi cha mwaka 2013/14 serikali imekusudia kuzalisha zaidi ya ajira 100,000 ili kukabiliana na tatizo la ajira nchini.
Kabaka alieleza pia katika mwaka ujao wa fedha, serikali itatengeneza ajira 300,000 mbali ya nyingine 61,915 zitakazopatikana kwenye sekta ya Utumishi wa Umma.
Alisema pia kwa kupitia programu yake ya miaka mitatu, 2013/14 hadi 2015/16 itatengeneza ajira 600,000 kwa vijana.
“Serikali imelenga kujenga uwezo wa vijana wa kupata ujuzi na stadi mbalimbali za kazi,” alisema Kabaka.
Alizitaja stadi hizo kuwa ni kuwapatia mitaji na mikopo nafuu, kuwatengea maeneo ya uzalishaji na biashara, kuwalinda kisera na kisheria.

Chanzo: Mwananchi